Sera ya mambo ya nje ya William Ruto: Je tutegemee nini?

Nico Minde
5 min readSep 15, 2022

Mara baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Kenya, William Ruto alianza kukutana na wawakilishi mbali mbali wa mataifa ya kigeni. Licha ya tashwishi ya uhalali wa ushindi wake Ruto, ambaye hadi uchaguzi mkuu alikuwa naibu wa rais, alianza kupokea ugeni mkubwa kutoka mataifa ya kigeni pamoja na kukutana na wawakilishi mbali mbali wa mashirika ya kimataifa. Mara baada ya kutangazwa kama rais mteule Ruto alipokea ugeni wa wawakilishi kutoka Marekani ukingozwa na senata wa Delaware Chris Coons. Ujumbe huu wa Marekani ulionyesha umuhimu wa Kenya kwenye anga za kiusalama, kiuchumi na kimkakati. Japo ujumbe huu wa Marekani pia ulikutana na rais Uhuru Kenyatta pamoja na mgombea urais Raila Odinga — kukutana kwao na Ruto kuliashiria imani yao na Ruto. Hii ni minghairi ya kwamba kulikua na fununu kwa wakati ule kwamba Raila Odinga atapinga matokeo mahakamani. Na hakika, Raila Odinga pamoja na wabia wake mbali mbali walifungua kesi kwenye mahakama ya juu ya Kenya kupinga ushindi wa Ruto.

President William Ruto. Photo courtsey.

Hata wakati kesi inaendelea Ruto aliendelea na mikakati ya kupanga serikali yake. Mahakama ya juu hatimaye ilimdhibitisha Ruto kama rais mteule na kutupilia mbali mashauri yote yaliyoletwa kwenye mahakama hio. Ushindi huu wa mahakamani ulishadidia ushindi wake kwenye uchaguzi japo wapinzani wake waliikosoa mahakama. Kisheria, maamuzi ya mahakama ya juu ni ya mwisho.

Tarehe 13 Septemba, Ruto aliiapishwa rasmi kuwa rais wa tano wa Kenya. Kwenye hafla ya uapisho, takribani marais ishirini na viongozi wa nchi mbali mbali walihudhuria. Kando ya viongozi hawa, nchi mbali mbali zilituma wawakilishi wao. Wafanyibiashara tajika Afrika pia walihudhuria sherehe hio akiwemo Aliko Dangote, ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes ndiye tajiri mkubwa Afrika. Mwingine aliyehudhuria ni Rostam Aziz, mfanyibiashara mkubwa Tanzania ambaye ni mbia kwenye kampuni ya Vodacom. Rostam Aziz ameonyesha nia ya kuekeza katika sekta ya gesi nchini Kenya. Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa akiwemo Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), wawakilishi wa Umoja wa Ulaya na mabalozi mbali mbali walishiriki katika hafla ya uapisho wa Ruto.

Katika hafla hiyo, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alipewa nafasi ya kuzungumza kama “Mzee” wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alizungumza akitoa salama za pongezi kwa niaba ya Jumuiya. Naye rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alizungumza. Katika hotuba yake Rais Museveni alitambua juhudi za Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alikuwa mmoja wa marais waliohudhuria. Kumekua pia na tetesi kwamba Ethiopia nayo inategemea kuomba uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed pia alihudhuria.

Mihimili ya diplomasia

Kulingana na mihimili ya sera ya kidiplomasia ya Kenya, ushirikiano wa kimataifa ni muhimu sana. Mihimili hii inajumuisha sera ya diplomasia ya uchumi, sera ya diplomasia ya kitamaduni, sera ya diplomasia ya mazingira, sera ya diplomasia ya amani pamoja na diplomasia ya diaspora. Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Ruto alisisitiza kuendelea kwa sera ya mambo ya nje kulingana na mihilimili hii. Mhimili wa amani umekuwa nguzo muhimu katika diplomasia ya Kenya. Hii inatokana na migogoro ya kisiasa inayokumba mataifa jirani ya Kenya.

Kenya imesimamia mazungumzo ya amani Somalia na Sudan (Sudan Kusini). Rais aliyemaliza muda wake Uhuru Kenyatta pia alijikita katika juhudi za amani kwenye mgogoro wa Tigray, Ethiopia. Novemba 2021, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alizuru Kenya na kufanya mazungumzo na rais Uhuru Kenyatta kuhusu mgogoro wa Ethiopia. Kabla ya ujio wa Blinken, rais Kenyatta alikua amekutana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed nchini Ethiopia. Diplomasia ya amani chini ya uongozi wa Kenyatta pia ulijikita katika mikutano ya kikanda kuhusu mgogoro wa mashariki mwa Congo. Kutokana na hayo, Rais Ruto ametambua mchango wa Kenyatta kwa kumwambia kwamba ataendelea na michakato ya amani kwenye ukanda wa maziwa makuu na pembe ya Afrika.

Diplomasia ya diaspora

Katika kuonyesha uzito wa ugeni uliokuwa umekuja ugani Kasarani, Ruto alitambua uwepo wao. Zaidi, Ruto alizungumzia kuimarisha uhusiano baina ya Kenya na wananchi wake waishio ughaibuni (diaspora). Ruto alitoa ahadi ya kuimarisha uhusiano huu wa kidiaspora na kuipa hadhi ya kiwizara. Takwimu zinaonyesha wanadiaspora wa Kenya wanachangia sana kwenye fedha za kutoka nje (remittances). Zaidi ya Kshs 283.6 billion zilitumwa nchini na Wakenya washio ughaibuni kati ya Januari na Julai mwaka huu. Katika hotuba yake alisema mchango huu usiishie tu kwenye masuala ya remittances bali pia michango mingine ikiwemo ushiriki kwenye masuala ya kupiga kura na ushiriki katika masuala ya kitaifa.

Katika hatua nyingine, Rais Ruto katika hotuba yake, aliahidi kuendelea na juhudi za kuimarisha uhusiano wa Afrika Mashariki. Alitambua ujio wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki mapema mwaka huu. Katika juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na biashara, Rais Ruto pia alisema Kenya itaendelea kushiriki kikamilifu katika kutekeleza makubaliano ya eneo huru la biashara na soko la pamoja barani Afrika (ACFTA). Pia alizungumzia suala la mabadiliko ya tabia nchi na kuhakikishia ushiriki wa Kenya kwenye mkutano wa tabia nchi Afrika Novemba mwaka huu.

Katika siku yake ya kwanza madarakani, Rais Ruto alikutana na marais na wawakilishi mbali mbali.

Mtanziko wa Jamhuri ya Sahrawi

Katika hali ya kushangaza, Rais Ruto alitoa agizo la Kenya kusitisha kuitambua Jamhuri wa Sahrawi (SADR) siku yake ya kwanza madarakani. Hii ni mara baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Nasser Bourita. Cha ajabu ni kwamba rais wa Sahrawi Brahim Ghali alihudhuria hafla ya uapisho wa Ruto. Katika hafla hio, Ruto alitambua uwepo wa rais Ghali na sio uwepo wa Waziri Bourita. Muda mchache baadae ujumbe wa kusitisha kuitambua SADR ulifutwa kwenye akaunti ya Twitter ya Ruto. Kenya ni baadhi ya nchi ambazo zimekua zikiitambua SADR na hata kuwakubalia kufungua ubalozi Nairobi mwaka 2014. Maaumuzi ya haraka ya Ruto bila hata kuwa na baraza la mawaziri linaonyesha udhaifu wa mapema kwenye diplomasia. Kwenye sera ya mambo ya nje, mara nyingi nchi hubaki bila upande mpaka pale maslahi yake yanaanishwa. Kitendo cha ‘kukurupuka’ cha Ruto sio kiashiria kizuri. Ikumbukwe katika kampeni zake, Ruto alitoa matamshi tatanishi dhidi ya Congo.

Taswira ya sera ya mambo ya nje ya Ruto

Msingi wa sera ya mambo ya nje ya nchi mara nyingi inakua endelevu na mageuzi yanakua kidogo kulingana na mitazamo binafsi ya kiongozi ambaye yuko madarakani. Ilani ya uchaguzi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Ruto kiliahidi sera ya mambo ya nje ambayo inayoegemea Afrika. Hatua muhimu itakayofuata katika kuanisha dira ya diplomasia ya Ruto itakua katika uteuzi wa waziri wa mambo ya nje.

Mtu atakayechaguliwa kuongoza diplomasia ya Kenya lazima awe mwenye uzoefu na tajriba ya kimataifa. Kuna minong’ono ya wizara hiyo kupewa watu kama Ababu Namwamba ambaye aliyekua naibu waziri wa mambo ya nje. Namwamba pia alikua mratibu wa mahusiano ya kimataifa kwenye kampeni ya Ruto. Mwingine anayetupiwa jicho ni Balozi Macharia Kamau, Katibu Mkuu kwenye wizara ya mambo ya nje. Balozi Kamau ana uzoefu mkubwa kwenye anga za kimataifa. Balozi Kamau alihudumu kama mwakilishi wa kudumu Umoja wa Mataifa.

Kenya imejijengea sifa kama taifa muhimu kwenye ukanda wa Afrika mashariki. Sifa hii inatokana na uimara wa uchumi wake na siasa zake imara. Rais Ruto anajukumu la kuendeleza umuhimu huu kwa mikakati madhubuti inayolenga kuimarisha maslahi mapana ya Kenya.

--

--

Nico Minde

God Given | Faith | Hope | Love | Academic | Interested; International Relations | Politics and Culture | Tanzania | Foreign Policy | Music and Performance